SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi
wa Umma imesema ipo tayari kuhakiki mali za Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda, endapo watapokea malalamiko kutoka kwa wanaomtilia
shaka.
Hivi karibuni wakati akitangaza orodha ya
watu wanaotuhumiwa kuuza, kuagiza na kutumia dawa za kulevya, Makonda
alijikuta akiingia katika vita ya maneno na wabunge.
Msingi wa vita yenyewe ni hatua ya baadhi
ya wabunge kupinga utaratibu alioutumia Makonda kuwataja kwa majina
watuhumiwa hao na hata kwenda mbali zaidi wakimtuhumu na kuhoji
alikopata utajiri wa ghafla.
Hatua ya kuhoji mali za Makonda
ilichochewa na kauli ya Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alionekana kukerwa na
ukosoaji wa wabunge hao na hivyo kuwatuhumu wawakilishi hao wa wananchi
kulala bungeni na kuitikia kila kitu ndiyoooo.
Akizungumza ili kupata ufafanuzi kwa
upande wa sekretarieti hiyo juu ya madai hayo ya utajiri wa Makonda na
iwapo aliziorodhesha kama sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya 1995
inavyoelekeza, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa sekretarieti hiyo,
Joseph Ishengoma, alisema chombo hicho kipo tayari kufanya uhakiki
endapo watapokea malalamiko rasmi kutoka kwa wananchi au wabunge
waliosikika hivi karibuni wakizungumzia suala hilo bungeni.
Alisema kinachotakiwa ni kufuata
utaratibu ambao ni kupeleka malalamiko kwa sekretarieti hiyo kuomba
kufanyika kwa uhakiki wa mali za kiongozi huyo kutokana na tuhuma
walizozitoa.
Kauli hiyo ya sekretarieti imekuja ikiwa imepita takribani wiki moja sasa tangu wabunge na Makonda washambuliane kwa maneno.
Miongoni mwa wabunge walioonekana kukerwa
na kauli pamoja na utaratibu alioutumia Makonda na hata kutaka naye
achunguzwe ni Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, ambaye
alikwenda mbali na kutaja mali zinazodaiwa kumilikiwa na Mkuu huyo wa
Mkoa wa Dar es Salaam.
Akichangia taarifa za Kamati za Bunge za
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,
Selasini alisema Makonda amenunua jengo (apartment) lenye thamani ya
shilingi milioni 600.
“Makonda amenunua apartment pale Viva
Towers kwa shilingi milioni 600, Makonda amempa mke wake gari aina ya
Mercedez Benz lenye thamani ya Dola 250 za Marekani (shilingi milioni
550) kama zawadi ya birthday,” alisema Selasini.
Siku moja kabla ya Selasini kusema hivyo,
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Rushaku (Msukuma), naye aliibuka na
tuhuma nyingine nzito dhidi ya Makonda na kutaka vyombo husika
vimchunguze.
“Mheshimiwa Spika, nasimama kwa kanuni
ya 68(7) kuhusu jambo lililojitokeza jana (juzi) wakati wa mjadala wa
Bunge…naomba mwongozo wako.
“Mimi binafsi naunga mkono jitihada za
Rais kukamata wauza dawa za kulevya, lakini dalili ya kwanza ya kuanza
kumhisi mtu kama anajishughulisha na biashara ambazo hazieleweki, kwanza
ni mwenendo wa mtu yeyote…si mbunge wala si nani.
“Anatumia Lexus ya petroli ya Sh milioni
400, lakini imekarabatiwa ofisi (yake) ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya
Sh milioni 400 bila kufuata utaratibu wa manunuzi wa Serikali.
“Ana ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la
ghorofa…ni kina nani wanaotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi? Na
hawa mawaziri tulionao humu kwanini wamepigwa ganzi? Utawala bora, Mambo
ya Ndani na Waziri wa Sheria…kwanini mmepigwa ganzi?”
Msukuma pia alihoji anakopata fedha
Makonda za kwenda Paris na Marekani na kukaa siku 21 hasa ikizingatiwa
kuwa tiketi moja ni Dola za Kimarekani 14,000 huku yeye na mkewe jumla
ikiwa ni dola za Kimarekani 28,000.
Kutokana na hilo, Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano wa Sekretarieti hiyo, Ishengoma, alisema wabunge hao baada
ya kutoa malalamiko ya kutilia shaka mali za Makonda, wanatakiwa kulipia
kiasi cha shilingi 1,000 na kisha watapewa faili kwa ajili ya kuangalia
na kujiridhisha mali ambazo Makonda alizitaja kwao.
Alisema na hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.
Alisema kwa kuzingatia Katiba na sheria
hiyo, Sekretarieti itakuwa na wajibu wa kupokea hati za tamko rasmi
zinazohitajika kutolewa na viongozi wa umma kwa mujibu wa Katiba au
sheria nyingine yoyote.
Alisema kifungu cha 18 (b) kinaeleza
kuwa; Sekretarieti itapokea malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa sheria
ya maadili ya viongozi wa umma kutoka kwa wananchi.
Kifungu cha 18 (c) Sekretarieti
itachunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa sheria ya maadili ya viongozi
wa umma na viongozi wote wa umma wanaopaswa kuwajibika chini ya sheria
hiyo.
Alisema pia sekretarieti katika
kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa vipengele hivyo, itakuwa na
mamlaka ya kupokea na kusikiliza malalamiko yote kuhusu kiongozi yeyote
wa umma yawe kwa mdomo au kwa maandishi kutoka kwa si tu wabunge hao
bali kwa mwananchi yeyote bila kuuliza majina na anwani za watu
waliopeleka malalamiko hayo.
Kwa mujibu wa sheria ya maadili ya mwaka
1995 (23) (1) endapo mtu mwenye wadhifa wa waziri au wa mkuu wa mkoa
amekiuka miiko hiyo malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa rais na mtu
yeyote kwa maandishi yaliyotiwa saini, anwani na jina la mlalamikaji.
Zaidi, Ishengoma alisema taarifa ya mali
za Makonda pamoja na viongozi wengine ziliwasilishwa katika ofisi yao
Desemba 31, mwaka jana kwa mujibu wa sheria.
Alisema pamoja na hayo hatamzuia mtu kupeleka kile anachokijua ili waweze kufanyia kazi.
“Sheria hii yenyewe inampa mtu
‘Comsumption’ kama Kamishna wa Tume ya Maadili ataangalia kama mali zake
zina ushahidi na ofisi inaweza kufanya uhakiki wa kupata taarifa sahihi
kama alificha hizo mali hapo awali au la na hatua ya kwanza atapewa
kubadilisha.
“Na kama Kamishna akiridhia kuwa
amedanganya basi atapelekwa katika Baraza la Maadili na anayelalamika
anakuwa ni miongoni mwa mashahidi na kitakachofuata atajitetea na
chombo hicho kitatoa mapendekezo,” alisema Ishengoma.
SELASINI ANENA TENA
Akizungumza kwa njia ya simu jana na
gazeti hili lililotaka kujua iwapo atapeleka malalamiko katika
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutaka kuhakiki mali za
Makonda kama alivyomtuhumu bungeni, Selasini ambaye yupo jimboni kwake
Rombo alisema hawezi kupeleka malalamiko kwa kuwa viongozi wengi ni
waongo.
Katika hilo wao wamekwishataja na kilichobaki ni vyombo vya uchunguzi kufanya kazi hiyo.
“Watu wamejaza mali zao majina ya shemeji
zao, wake zao, watoto wao, mahawara zao hivyo kupeleka malalamiko sisi
ni kujidanganya tu.
“Sisi tumeshasema na si lazima tupeleke
malalamiko, hapa kinachotakiwa ni vyombo vya uchunguzi vifanye kazi
zake, kwani havina watu wa kuchunguza kuanzia safari ya Ufaransa siku 21
kwa kwenda Airport kuchunguza alivyoondoka,” alihoji Selasini.
Alisema hakuna haja ya vyombo vya
uchunguzi kutupia aliouita mzigo kwa watu wengine huku akisema endapo
atapeleka malalamiko shahidi atatakiwa awe yeye mwenyewe na hana muda wa
kupoteza katika hilo.
Alisema siku ambayo alimtuhumu Makonda
kumiliki mali hizo alipomaliza tu na kutoka alifuatwa na mtu aliyemtaja
kuwa wa usalama na kumweleza kuwa Makonda Dodoma ana viwanja 19 na vipo
kwa jina lake.
“Hilo nalo watataka tupeleke malalamiko,
hapana wanatakiwa kufika tu Ardhi Dodoma na kuangalia jinsi ambavyo
alivyoviandikisha vyote kwa majina yake, lakini kwa kupeleka malalamiko
hatutafika katika hili na hutampata mtu, vyombo vya uchunguzi vifanye
kazi yake tu,” alisema Selasini.
Alisema kuundwa kwa chombo hicho lengo
lake nikuwa na viongozi wenye maadili hivyo kama watashindwa kufanya
hivyo itakuwa ni kwa sababu ya kuingia katika siasa.
MSUKUMA
Alipotafutwa Msukuma kuelezea kama ana nia ya kupeleka malalamiko, alisema hiyo si kazi yake.
“Hizo ni kazi za Spika wa Bunge yeye
ndiye anatakiwa kunipigia simu na kuniambia nipeleke malalamiko au
wanipe maelekezo nifanye hivyo na si mwandishi,” alisema na kukata simu
ghafla.
No comments:
Post a Comment