CHAMA Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimesema dhana ya kuanzishwa kwa fikra ya Umoja wa kitaifa
ilianzia kwa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid
Aman Karume, na sio ajenda ya vyama vya upinzani.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar Dkt. Abdallah Juma Abdallah “Mabod”
wakati akizungumzia historia ya maisha ya Mwasisi wa ASP ambayo ni CCM
kwa sasa Marehemu Mzee Karume huko Afisini kwake Kisiwandui Unguja.
Amesema Mwasisi huyo alikuwa ni
kiongozi anayepinga utengano na ubaguzi misingi ya kidini, kikabila na
kisiasa ndio maana katika Baraza la mwanzo la Mawaziri kupitia Baraza la
Wawakilishi la Wakati huo aliteuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya
upinzani ili kujenga Umoja wa kitaifa na kuondosha ubaguzi.
Aidha alisema kuwa viongozi
walioteuliwa kutoka vyama vya upinzani walikuwa ni waadilifu waliofuata
miongozo na matakwa ya serikali kwa wakati huo licha ya kujitokeza kwa
vitendo vya usaliti kwa viongozi hao.
“ Mzee karume alikuwa na moyo wa
huruma na akiwapenda wananchi wa visiwa vya Zanzibar wawe na maendeleo
endelevu.”, alisema Dkt. Mabodi.
Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza
kuwa lengo la kufanyika kwa Mapinduzi ya Mwaka 1964, lilikuwa ni
kurejesha heshima ya wazawa waliotawaliwa kimabavu na utawala wa
Kisultani kwa zaidi ya miaka 100.
Alisema baada ya mapinduzi hayo
Marehemu Mzee Karume na Jopo lake la Umoja wa Vijana wa ASP, waliweka
mipango mikakati ya kuimarisha maendeleo ya Zanzibar.
Pia aliweka vipaumbe mbali mbali
vikiwemo kuanziasha mpango wa kuboresha Sekta ya Elimu na Afya kwa
kuwapeleka vijana mbali mbali nje ya nchi ikiwemo China, Urusi, Cuba na
mataifa mengine ili wapate utalamu wa fani tofauti zikiwemo Udaktari na
masuala ya Uongozi ili kuharakisha maendeleo ya nchi.
Hata hivyo aliweka mfumo wa Elimu
bure ili Watoto wa Kiafrika waliokuwa hawana fursa ya kusoma wakati huo
wajifunze na kuelimika ili waweze kusaidia katika masuala mbali mbali ya
kiutendaji.
Dkt. Mabodi alisema kuwa Mzee
Karume alikuwa ni kiongozi jasiri na asiyetaka kukaa Ofisini bali
alikuwa akitembea maeneo mbali mbali na kujionea mwenyewe changamoto
zinazowakabili wananchi, tofauti na baadhi ya viongozi wa sasa
wanaosubiri taarifa za utekelezaji ofisini.
Hata hivyo alisema Mzee Abeid
Amani katika Harakati za kupinga ubaguzi ambao ulikuwa umejenga ngome,
enzi za utawala wa kifalme aliwatangazia wananchi kuwa wanatakiwa kuoana
makabila mbali mbali ili kuchanganya rangi kwa lengo la kufuta ubaguzi
uliokuwa kukisambazwa na watu waliokuwa ni miongoni mwa Waliopinduliwa.
Aidha alisema Mzee Karume pamoja
na mambo mema aliyoyafanya enzi za uhai wake pia ni mwasisi wa kwanza wa
Demokrasia kwani aliwakaribisha mataifa mbali mbali kuja Zanzibar
kuwekeza na kushauri masuala ya Kisiasa.
Aliimarisha miundombinu ya
barabara na kujenga nyumba za kisasa ambazo hivi sasa zinajulikana kama
nyumba za maendeleo Unguja na Pemba.
Pia aliimarisha Sekta ya
Mawasiliano kwa kuanzisha Televisheni ya mwanzo ya rangi Afrika
Mashariki na kati iliyoitwa TVZ ambayo kwa sasa ni ZBC TV, sambamba na
radio ya kisasa ya Sauti ya Tanzania Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliweka
wazi kuwa kiongozi huyo ametenda mengi mazuri kwa nchi ya Zanzibar,
hivyo viongozi na watendaji wa sasa waendeleze mambo mema yaliyoachwa
huku nao wakibuni vitu vingine vipya vinavyoendana na wakati uliopo
sasa.
Pia alimpongeza Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kufanyia
kazi kwa vitendo kauli mbiu ya “ Zanzibar kujitawala yenyewe kielimu,
kiafya na kimiundombinu ya kisasa” huku ikipiga vita adui ujinga na
maradhi.
Pamoja na hayo alimpongeza pia
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa
msimamo wake wa kulinda Muungano wa Serikali mbili na Mapinduzi ya
Zanzibar mambo ambyo ndio urithi wa Waasisi wa ASP na TANU wakiwemo
Marehemu Mzee Karume na Hayati Mwl. Nyerere.
Pamoja na hayo aliwambia wananchi
kuwa kila ifikapo April 7 ya kila mwaka ni maadhimisho ya kumbukumbu ya
siku ya mashujaa wa Zanzibar na waasisi wote waliofariki , na sio
sherehe ndio maana panafanyika hitima na kuombwa dua kwa lengo la kuenzi
juhudi zao.
No comments:
Post a Comment