Z4news blog
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunasikitishwa na mlolongo wa
matukio ya uvunjifu wa amani yanayoshamiri siku hadi siku. Kituo
tunashitushwa na matukio hayo yanayodunisha amani na kumomonyoa misingi
ya demokrasia nchini Tanzania.
Tukio la uvamizi katika mkutano wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF)
uliopelekea kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na waandishi wa habari
huko Mabibo, Ubungo, Dar es Salaam limezidi kuzua mjadala katika jamii
juu ya hatma ya hali ya usalama kwa taifa. Tunatoa pole kwa waandishi wa
habari, viongozi na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF).
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaona kuwa huu ni ukiukwaji
mkubwa wa misingi ya demokrasia kwa kuzingatia aina ya shughuli
iliyokuwa ikiendelea. Pia tukio hilo limezua hofu juu ya usalama wa
wanahabari wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo
linazorotesha haki ya kupata taarifa.
Tunaitaka serikali kutofumbia macho matukio haya yanayoota mizizi kwani
kwa kufanya hivyo ni kuhalalisha vitendo vya kihuni na kuruhusu
uvunjwaji wa sheria kiholela.
Kwa kuzingatia umuhimu wa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika
kituo cha sheria na haki za Binadamu tunapendekeza yafuatayo;
Msajili wa vyama vya siasa kuhakikisha ustawi mzuri wa vyama vya siasa
kwa kutatua migogoro iliyopo ndani na baina ya vyama vya siasa ili
kuepusha matukio ya uvunjifu wa amani na kudumisha ustawi wa demokrasia.
Serikali kuhakikisha usalama kwa raia wanapokuwa kwenye shughuli zao ili kuepusha hofu kwa wananchi.
Vyama vya siasa kutumia uhuru wao kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa bila kusababisha uvunjifu wa amani.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunataamali jamii yenye kuheshimu na kulinda haki za binadamu.
Imetolewa na:
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaj
No comments:
Post a Comment