Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, alifanya ziara ya
kikazi jijini Seoul, jamhuri ya Korea tarehe 24 Aprili 2017 kwa mwaliko
kutoka kwa Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya
Korea. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25
tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na
Jamhuri ya Korea mwaka 1992.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri
ya Korea, Mhe. Yun Byung-se
Katika taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, Mheshimiwa
Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Yun
Byung-se ambapo Waziri Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea
kwa kumpatia mwaliko wa kutembelea taifa hilo, hususan wakati huu
inapoadhimishwa jubilee ya miaka 25. Mhe. Mahiga aliishukuru Serikali ya
Jamhuri ya Korea kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kimkakati katika
uwekezaji kwa kipindi cha kuanzia 2016 -2020.
Kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania
kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo,Ujenzi wa Daraja la
Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla
ya urefu wa mita 275, pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa
48; Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa
600 imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali,
vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI,
CT-Scan, mashine maalum kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake.
Vilevile, Ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto Chanika, yenye uwezo
wa kulaza wagonjwa 160 inatarajiwa kufunguliwa siku za karibuni.Aidha,
Watanzania zaidi ya 1000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma
katika vyuo mbalimbali vya Jamhuri ya Korea.
Waziri Mahiga pia alikutana na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya
wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza
fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania mathalani ujenzi wa Reli ya Kati
katika viwango vya kimataifa; uzalishaji na usambazaji wa nishati ya
umeme; ujenzi wa maeneo ya viwanda; na huduma ya kutoa ushauri katika
miradi mikubwa.
Aidha, Mhe. Waziri aliwahakikishia wawakilishi wa makampuni ya
Jamhuri ya Korea kuwa, Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji na
biashara pamoja na taasisi muhimu zinazotoa huduma mbalimbali katika
sekta hiyo.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo kukutana na
Balozi Sul Kyung-hoon Makamu wa Rais wa KOICA ambapo aliishukuru Taasisi
hiyo kwa kuipatia zaidi misaada Tanzania kwa uwazi na bila ya masharti
yeyote. Pia aliipongeza KOICA kwa kushirikisha jamii kuanzia wakati wa
ubunifu wa mradi hadi kufikia utekelezaji pamoja na usimamizi. KOICA
wameombwa kuongeza maeneo ya misaada na kujumuisha maeneo ya ujenzi wa
miundombinu ya maji na nishati ya umeme wa jua, upepo na maji kwa ajili
ya kusaidia maeneo ya vijijini. Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alishauri
KOICA kuangalia uwezekeno wa kuanzisha vituo vya kilimo cha kisasa,
vituo vya kufugia na vituo vya kufundisha ujasiriamali ili jamii kubwa
ya Watanzania iweze kunufaika.
Katika jitihada za kutafuta washirika kwa ajili ya kusaidia kuboresha
Chuo cha Diplomasia, Mhe. Waziri akiwa Seoul alitembelea Chuo cha Taifa
cha Diplomasia cha Jamhuri ya Korea na kufanya mazungumzo na Balozi
Paik Ji-ah, Kaimu Mkuu wa Chuo. Lengo kuu lilikuwa kujifunza uendeshaji
wa Chuo, mitaala iliyoandaliwa kutoa masomo, walengwa wa masomo hayo,
aina ya wakufunzi, lugha zinazotumika kufundishia, utaratibu wa kuandaa
wanadiplomasia na mifumo ya chuo hicho.
Vilevile kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mhe. Waziri alikutana na
Jumuiya ya Watanzania waishio Jamhuri ya Korea ambapo aliwahimiza
kuheshimu sheria na taratibu za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta
utaalam utakaosaidia kuiendeleza Tanzania.
Mhe. Waziri aliwasihi Watanzania waliopo huko ambao ni wanafunzi
kuzingatia masomo ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta faida kwa
familia zao na taifa kwa ujumla. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri
aliwahakikishia Wanajumuiya hao kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho
za kufungua Ubalozi wa Tanzania jijini Seoul na kuwaomba kutoa
ushirikiano kwa Balozi wa kwanza wa Tanzania katika nchi hiyo
No comments:
Post a Comment