Waziri wa Nchi Ofisi Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.George Simbachawene akitoa taarifa kwa
vyombo vya habari kuhusu uchaguzi na upangaji wa wanafunzi wa kujiunga
na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2017.
Waziri wa Nchi Ofisi Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.George Simbachawene akizungumza juu ya
taratibu za Uchaguzi wa Wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na
Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2017.
……………………………….
WAZIRI wa ofisi ya Rais Tawala za
mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene amesema Jumla
ya wanafunzi 93,019 ndiyo waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano
pamoja na vyuo vya ufundi kwa mwaka wa masomo wa 2017.
Simbachawene ametoa taarifa hiyo
jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa
kutangaza matokeo ya wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2016 na
kufaulu kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi mwaka
huu.
Alisema kuwa kati ya wanafunzi
96,018 ni wanafunzi 93,019 ndiyo wenye sifa za kuchaguliwa kujiunga na
kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi kwakuwa wamefaulu vigezo vyote
vya msingi.
“Kati ya wanafunzi hao 92,998 ni
wa shule (School Candidates) na wanafunzi 21 walisoma chini ya taasisi
ya elimu ya watu wazima”alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa jumla ya watahiniwa
wa shule 349,524 wakiwemo wasichana 178,775 sawa na asilimia 51.1 na
wavulana 170,749 sawa na asilimia 48.9 walifanya mtihani huo mwaka 2016.
“Watahiniwa wa kujitegemea
waliofanya mtihani huo wa mwaka 2016 walikuwa 47,751 wakiwemo wasichana
24,587 sawa na asilimia 51.5 na wavulana 23,164 sawa na asilimia
48.5”alifafanua Simbachawene.
Alisema kuwa watahiniwa waliofaulu
kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu ni 96,018 sawa na asilimia 27.60
ya watahiniwa waliofanya mtihani Tanzania Bara hivyo kufanya ufaulu
kuongezeka katika mwaka 2016 kwa asilimia 3.15 ukilinganishwa na mwaka
2015.
Alisema kuwa kwa mwaka 2017
uchaguzi na upangaji wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo
vya ufundi umezingatia mwongozo wa Wizara ya elimu , Sayansi na
Teknolojia wa tarehe 15 mei 2017 na hakuna fursa ya kufanya mabadiliko
yoyote ya shule.
“Mwongozo huu unalenga kwamba,
kigezo cha mwanafunzi kujiung na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni
AAA hadi CCD kama cut off point kwenye masomo ya tahasusi na pili
Crediti 3 na pointi zisizopungua 25 kwenye daraja, machaguo yaliyojazwa
na mwanafunzi kwenye selform yake na mwisho nafasi zilizopo katika shule
husika”alifafanua.
Aidha aliwataka wanafunzi wote
waliochaguliwa kuripoti katika shule walizopangwa kwa wakati, endapo
watachelewa kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya kufungua shule nafasi
zao itachukuliwa na mwingine.
“Tarehe ya kuripoti katika muhula
wa kwanza kwa kidato cha tabo kwa mwaka 2017 utaanza tarehe 17 july 2017
lakini kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha sita watafungua tarehe 3
july 2017 kama ilivyokuwa imepangwa”alisema.
Hatahivyo aliwaagiza watendaji wa
wilaya na mikoa pamoja na wadau wa elimu nchini kuhakikisha miundombinu
ya shule ikiwemo maabara na majengo mengine muhimu yanakamilika ili
yaweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.
No comments:
Post a Comment