Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri
ya Manispaa ya Ubungo – Kata ya Ubungo alipofanya ziara ya kikazi
katika Kata hiyo ili kupokea maoni, ushauri na kusikiliza kero za
watumishi wa umma leo Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya watumishi wa umma wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo – Kata ya Ubungo wakimsikiliza Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) (Hayupo pichani) wakati wa kikao
kazi na watumishi hao kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu
wa Taasisi ya Maji (Water Institute), Dkt. Shija Kazumba akiwasilisha
hoja mbalimbali zinazowahusu watumishi wa umma kutoka taasisi
anayoiongoza wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo – Kata ya
Ubungo kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akifafanua hoja mbalimbali alizopokea
kutoka kwa watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo –
Kata ya Ubungo (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi na watumishi hao
leo Jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe.
Kisare Makori na kushoto kwake ni Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe.
Boniface Jacob.
………………………………………………………………………….
Mamlaka za ajira katika utumishi
wa umma nchini zimeelekezwa kufanya marekebisho ya taarifa za watumishi
wa umma wanaotarajiwa kustaafu ili waweze kupata stahili zao kwa wakati
kama inavyostahili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki
(Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo – Kata ya Ubungo, jijini Dar es
Salaam.
Mhe. Kairuki amesema wapo
watumishi wa umma ambao walipandishwa vyeo lakini muda wao wa kustaafu
umekaribia na bado hawajafanyiwa mabadiliko yoyote katika taarifa zao.
“Natumia fursa hii kuwaelekeza
waajiri wote katika utumishi wa umma warekebishe taarifa za watumishi
hawa wanaokaribia kustaafu ili waweze kupata haki na stahili zao,” Mhe.
Kairuki amesema serikali inawajali watumishi wa umma na kuongeza wale
ambao tayari wameshastaafu, watafutwe na wajaze fomu maalum za madai
kupitia kwa waajiri wao ili serikali iwalipe stahili zao kadri
inavyostahili.
“Nawaagiza waajiri kupitia kwa
Maafisa Utumishi wao, wawatafute ili waweze kujaza fomu maalumu na
kuweza kupata haki zao kwani Serikali ipo kwa ajili ya watu wote hivyo
hakuna haki ya mtumishi wa umma yeyote itakayopotea,” Mhe. Kairuki
amesema.
Mhe. Kairuki amewata watumishi wa
umma kutimiza wajibu wao kwa weledi ili kuboresha utendaji kazi.
“Serikali ni mimi na wewe hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kutimiza
wajibu wake ipasavyo ili kujenga uchumi wa nchi yetu”.
Awali, akimkaribisha Mhe. Kairuki
kuzungumza na Watumishi wa Kata ya Ubungo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,
Mhe. Kisare Makori amempongeza Mhe. Waziri Kairuki kwa utaratibu
anaoufanya wa kukutana na watumishi wa umma kwa kusikiliza maoni pamoja
na changamoto wanazozikabili katika utendaji kazi na kuzifanyia kazi.
“Kinachofanyika sasa ni jambo la
kipekee sana kwa Waziri Kairuki mwenye majukumu mazito kutoka ofisini
kwake na kuja kuzungumza katika kikao kama hiki na watumishi wa umma,
kwa niaba ya viongozi wenzangu wa Wilaya ya Ubungo, nampongeza sana,”
Mhe. Makori amesema.
Mhe. Makori amewataka watumishi
wa umma wa Ubungo kuitendea haki ziara ya Waziri Kairuki kwa kutekeleza
maagizo yote yanayotolewa.
Mhe. Kairuki yupo katika ziara ya
kikazi katika mkoa wa Dar es salaama ambapo leo ni siku ya saba akiwa
katika Kata ya Ubungo kwa kukutana na watumishi wa umma wa kada zote
katika vikao kazi.
Lengo la kukutana na watumishi wa
umma ni kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili
katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta
mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo
yaliyopangwa na Serikali.
No comments:
Post a Comment