WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepiga marufuku viongozi wa Serikali kufanya biashara ya pembejeo na
vishada kama hawana mashamba ya tumbaku.
“Kuna baadhi ya viongozi wa
Serikali hapa mkoani wamejiingiza kwenye biashara ya vishada na uuzaji
wa pembejeo. Hii ni dosari. Hatutaruhusu hili hata kidogo,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa onyo hilo jana
jioni (Jumatano, Agosti 9, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao la
tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na
Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi,
mjini Tabora.
Alisema: “Kiongozi wa Serikali ni
lazima uwe shamba na ulilime kisasa ili liwe ni shamba darasa kwa
wakulima walio jirani nawe. Usifanye biashara ya pembejeo kana huna
shamba. Nanyi viongozi wa AMCOS msikubali kuuza vishada vya viongozi wa
Serikali, tukikukamata, utaenda jela.”
Alisema endapo viongozi wataamua
kulima mashamba ya zao hilo, watalazimika kujiunga na vyama vya msingi
(AMCOS) vya kwenye maeneo yao ili waweze kuuza kupitia huko kutokana na
agizo la Serikali linalokataza makampuni kununua tumbaku bila kupitia
kwenye vyama vya msingi.
Aprili 15, mwaka huu, akiwa
katika ziara ya siku moja mkoani Tabora, Waziri Mkuu aliagiza wakulima
wa kujitegemea (Indepenent Farmers) na wale wa kwenye vikundi
(Associations) wote wauzie tumbaku yao kupitia kwenye vyama vya ushirika
ili kuzuia utoroshaji wa zao hilo na wakulima wasio na madeni
kulazimika kuwalipia wenzao.
No comments:
Post a Comment