• Breaking News

    ..

    ..

    Saturday 30 September 2017

    China yaipatia Tanzania msaada wa fedha kusaidia sekta ya elimu

    Serikali ya China imeipatia Tanzania msaada wa Shilingi bilioni 29.4 kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu ya ufundi stadi, utalii wa kijiolojia na kukarabati wa Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

    Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa pili kulia) na Kaimu Balozi wa China Nchini Tanzania, Mhe. Gou Haodong (wa tatu kushoto) wakisaini makubaliano ya msaada wa Sh. bilioni 29.4 kwa ajili ya miradi ya Ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoani Kagera, Utalii wa Kijilojia na Ukarabati wa Uwanja wa Taifa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam. Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Fedha na Mipango
    Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou Haodong.
    Bw. Doto James alisema kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 22.4 cha msaada huo kitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA wilayani Ngara mkoani Kagera, ambacho kitakapo kamilika kitadahili zaidi ya wanafunzi 400.
    “Fedha hizo zitatumika kujenga vyumba 19 vya madarasa, ujenzi wa karakana 9 za kutolea mafunzo ya elektroniki, ufundi bomba, useremala, ufundi uashi na upakaji rangi” alisema Bw. James
    Alieleza kuwa kiasi hicho pia kitatumika kujenga majengo ya utawala, mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine itakayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo hicho.
    “Tunaamini kwamba msaada huo utakuwa sehemu ya kusaidia jitihada za Serikali za kujenga uwezo wa wataalamu wake watakaochangia kukuza sekta ya uzalishaji na hatimaye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini” alisema Bw. James
    Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James alibainisha kuwa katika makubaliano ya msaada huo, Jamhuri ya watu wa China, itatoa kiasi cha shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya kuukarabati Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Dar es Salaam.
    “Katika makubaliano yetu ya msaada wa kuendeleza Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000, China itatoa msaada wa kiufundi na vifaa vya kisasa vya michezo na utaalamu katika usimamizi na ukarabati wa uwanja,” alifafanua Bw. James
    Bw. Doto James alisema kuwa kiasi kingine cha shilingi  milioni 300 kitatumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa aina mpya ya utalii ujulikanao kama utalii wa kijiolojia “Geopark Project” katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, mkoani Arusha.
    Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na maajabu mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini ambayo hayajatumika kikamilifu kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa
    “Tanzania ina kila sababu ya kujifunza kutoka katika Hifadhi ya Kimataifa ya Jiolojia ya Jiaozuo ya Yuntaishan ya China, iliyoanzishwa mwaka 2000 ambayo inaongeza asilimia 37.2 ya watalii kila mwaka na huchangia asilimia 12 ya pato la Taifa la nchi hiyo” aliongeza Bw. Doto James.
    Aliishukuru China kwa ushirikiano wake wa dhati na Tanzania tangu miaka ya 1960 na kwamba mpaka sasa nchi hiyo imeendelea kuipiga jeki Serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi, Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI