Waziri mkuu Kassim Majaliwa
akisalimiana na mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,wakati
alipowasili katika kiwanda cha kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo
Pichandege Kibaha Mjini.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa
akisalimiana na mkurugenzi wa viwanda vya kutengeneza sabuni cha KEDS
Pichandege Kibaha Mjini ambae pia ni mkurugenzi wa kiwanda cha
kutengeneza vigae cha Twyford kilichopo Pingo Chalinze,Jack Feng.
Picha na Mwamvua Mwinyi
………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WAZIRI mkuu,Kassim Majaliwa
amezitaka serikali za vijiji na ngazi nyingine mkoani Pwani,kujikita
kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya viwanda ili
kulinda mali na usalama wa wawekezaji na watanzania kijumla.
Amesema haijajulikana hadi sasa
nia na dhamira ya watu wasiojulikana wanaojihusisha kupoteza maisha ya
watu ,na ni hatari endapo watajiingiza katika maeneo ya uwekezaji kwani
hakuna mwenye uhakika wa azma yao.
Aidha Majaliwa ,ametoa wiki mbili
kwa waziri wa maji kutathmini matokeo ya mwenendo wa mradi wa maji wa
WAMI ,ili kutoa utaratibu na kama sheria inaruhusu kuvunja mkataba ikiwa
mkandarasi ameshafikia kiwango cha asimilia 50 ya utekelezaji.
Waziri huyo ,pia ameziagiza
halmashauri nchini kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua
magari ya zimamoto yatakayosaidia kudhibiti majanga ya moto yanapotokea
hususan kwenye maeneo ya uzalishaji na viwanda.
Katika hatua nyingine amelitaka shirika la umeme
Tanesco,Dawasco kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya umeme na maji katika maeneo yenye uwekezaji ili kuvutia wawekezaji.
Alitoa rai hiyo,wakati wa ziara
yake ya siku moja ,aliyoifanya mkoani Pwani kutembelea kiwanda cha
kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo Kibaha,na cha kutengeneza vigae
Twyford Ceramics Ltd/Pingo,Chalinze ,Bagamoyo.
Majaliwa ,alieleza kuwa ni lazima raia mmoja mmoja na jukumu la kila mmoja kusimamia kulinda nchi kuanzia maeneo wanayoishi .
Alisema serikali imejipanga
kuendelea kusimamia amani na utulivu,ambapo amewataka wananchi waiunge
mkono serikali kupambana na wahalifu wasio na nia njema na serikali.
“Hatuna uhakika kwa watu hawa
wanaofanya vitendo vya ovyo,watanzan ia waungane na serikali,kupambana
ili wasije kuingia kwa wawekezaji na kupoteza ndoto za serikali za
kupata wawekezaji “alisema Majaliwa.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa maji ,alisema mradi wa WAMI ulikuwa ukamilike tangu mwezi July mwaka huu.
Alisema alitembelea mradi huo
mwezi juni mwaka huu ukiwa chini ya asilimia 38 na kusema mkandarasi
akiendelea kusuasua watamfukuza na kutoa agizo ikifika mwezi huu wafikie
asimilia 80.
“Nilitaka kuja mwezi huu lakini
nikaambiwa speed ni ndogo na bado hali hairidhishi,na mkandarasi
hajamaliza”mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amekuwa akiuliza juu ya
kukwama kwa mradi huo” ;”Nimetoa wiki mbili kwa waziri aangalie dhamana
ya kampuni kwenye ubalozi wao wa India na kuangalia sheria namna ya
kufanya ama kukamilisha mradi kwa muda mfupi uliobaki”alifafanua.
Kuhusu nishati ya umeme
Majaliwa,alisema serikali ipo mbioni kutekeleza mradi mkubwa wa umeme
stiegler’s gorge katika chanzo cha mto Rufiji, utakaozalisha megawatts
2,100 zitakazoondoa kama si kumaliza upungufu wa umeme uliopo.
Aliitaka halmashauri ya Chalinze,ijipange kwa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji.
Kuhusu suala la zimamoto ,Majaliwa
alisema mkoa huo kwasasa una viwanda vikubwa hivyo wakati serikali
ikipokea changamoto ya uhaba wa vifaa na magari ya zimamoto ,halmashauri
ijipange kupitia bajeti zao.
“Viwanda hivi ni vikubwa
vinajengwa ,kiwanda hiki cha KEDS kina jengo hilo hapo lenye urefu wa
mita 30 juu,tuombe mungu moto usitokee ,unawezaje kuzima moto kwa maji
ya kwenye ndoo ,ipo haja ya kuangalia namna ya kutatua changamoto hii”
“Dar es salaam ambako ni mji wa
kibiashara serikali itasaidia katika kununua mitambo ya kusaidia kuzima
moto kutegemea ukubwa wa majengo yaliyopo”aliongeza Majaliwa.
Kwa upande wa miundombinu ya
barabara,alitoa rai kwa halmashauri ya Mji wa Kibaha kuboresha barabara
zilizopita mitaani na kuhakikisha mitaa yote iwe na barabara bora kwa
kufumua zisizofaa na kuchonga barabara zenye viwango.
Pamoja na hayo ,Majaliwa alibainisha uwekezaji kama huu
unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya
Viwanda ambapo itaongeza pato la nchi na itazalisha ajira kwa wingi.
Aliwasihi vijana ambao tayari wana ajira kwenye viwanda hivyo kutumia nafasi walizozipata kwa kuchapa kazi .
Majaliwa aliwaomba vijana hao
kuchapa kazi na kuwathibitishia wawekezaji kuwa watanzania ni wachapazi
na wana uwezo wa kufanyakazi viwandani na hakuna haja ya kuleta
watumishi nje ya nchi.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,alimwambia
waziri mkuu ,kwamba mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya
barabara isiyo ya kuridhisha kwa wawekezaji.
Alitaja changamoto nyingine kuwa
ni upungufu wa nishati ya umeme isiyokidhi mahitaji kwani kwasasa
mahitaji ni megawatts 73.2 na uliopo ni megawatts 40 ambao bado
hautoshelezi.
Mhandisi Ndikilo,alieleza tatizo
la uhaba wa vifaa,vitendea kazi na magari kwa idara ya zimamoto na
kuhofia endapo janga la moto likitokea kushindwa kuzima moto kwa wakati
na kusababisha athari kubwa.
Mbunge wa jimbo la Chalinze
Ridhiwani Kikwete ,alilalamikia uzembe na uvivu uliokubuhu katika
utekelezaji wa mradi wa maji Chalinze (CHALIWASA).
Alielezea kuwa,tatizo la maji limedumu kwa takribani miaka 13 sasa hali inayosababisha adha kwa wawekezaji na wananchi kijumla.
Ridhiwani alisema ,haridhishwi na
mwenendo wa mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi huo
kutokana na kasi yake kuwa ni ndogo na haiendani na maagizo aliyoyatoa
waziri mkuu hapo awali.
Akiwa kiwanda cha KEDS ,mbunge wa
jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka ,alimuomba Majaliwa kuangalia kwa
jicho la tatu kero ya miundombinu isiyo rafiki kwa wawekezaji.
Koka alisema wawekezaji wengi
wanakimbilia kuwekeza mji wa Kibaha na mji huo upo usoni mwa barabara
kuu ya Morogoro-Dar es salaam lakini bado kuna tatizo la barabara mbovu.
Wakati huo huo ,mkurugenzi mkuu wa
kiwanda cha KEDS na Twyford ,Jack Feng alisema asilimia 95 ya malighafi
itakuwa inatoka hapa nchini .
Alisema katika kiwanda cha KEDS wameshaajiri watu 200 huku wakitarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 katika kiwanda hicho .
‘Ndani ya ujenzi huu kuna kiwanda
kingine kikubwa ambacho tutazalisha bidhaa ya pempars na kiwanda kingine
tutatengeneza misumali”alieleza Feng.
Alisema hatua ya ujenzi ni nzuri
imefikia asilimia 90 na wanategemea kuanza uzalishaji mwezi ujao,na
utagharimu dola mil.200 hadi utakapokamilika.
Feng alifafanua,kwenye kiwanda cha
Twyford watarajia kuajiri wafanyakazi 4,000 hadi 6,000 mara
watakapoanza kuzalisha mwezi Nov mwaka huu,sasa kuna wafanyakazi 1,200.
Mkurugenzi huyo ,alieleza gharama
ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Twyford ni dola mil. 56 sawa na
bilioni 120 na watauza vigae ndani ya nchi hadi nje ya nchi Zambia,
Uganda, Rwanda na Burundi
No comments:
Post a Comment