MKE wa rais mstaafu ,mama
Salma Kikwete ,akiwa katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike kimkoa
Mkoani Pwani yaliyofanyika Kibaha na kufadhiliwa na shirika lisilo la
kiserikali la Room To Read linalotekeleza mradi wa kumwendeleza mtoto wa
kike.
Picha na Mwamvua Mwinyi
……..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKE wa rais mstaafu ,mama Salma
Kikwete,amesema mkoa wa Pwani upambane na mafataki wanaoteka fikra za
watoto wao wa kike ili kuondokana na mimba za utotoni ambapo mkoa huo ni
kati ya mikoa kumi inayoongoza kwa mimba hizo kitaifa.
Aidha amekemea tabia inayofanywa
na mashuga dadi wanaojiona mahodari wa kutongoza na kunyemelea watoto wa
kike wanafunzi na wengine kuwakatisha masomo kwa kuwatia mimba na kudai
anaejiona hodari wa kutongoza dunia aende kwa wanawake wakubwa huko
mitaani.
Pamoja na hilo,Mama Salma
,ameitaka jamii kuachana na mila na desturi zinazochochea mimba ,na
kusema lazima zitazamwe ili kuwawezesha watoto hao waendelee na masomo
yao.
Aliyasema hayo,wakati wa
maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike kimkoa,yaliyofanyika wilayani
Kibaha mkoani Pwani,ambayo yamefadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali
la Room To Read.
Alisema mkoa unaoongoza kwa mimba
za utotoni ni mkoa wa Katavi wenye asilimia 45 ambapo mkoa wa Pwani upo
ndani ya mikoa kumi inayoongoza kwa mimba hizo ukiwa na asilimia 30.
Mama Salma alisema,mimba za
utotoni hazikubaliki ,watoto wa kike wajitambue , na wajijue wao ni lulu
,na thamani ya mtoto wa kike ni kufunga mapaja,wafunge mapaja yao na
wakifunga mapaja hakuna mdudu atakaeingia.
“Situmii kitu kinachoitwa tafsida
hapa,naongea kama ilivyo ili mzidi kunielewa na walengwa yawaingie
kikamilifu kichwani mwao”,alisema mama Salma.
Alisema ni wakati wa mkoa huo kuongoza kielimu na kuwa kumi bora kitaaluma badala ya kuongoza kwenye mimba za utotoni.
Hata hivyo Mama Salma alieleza
kwamba,tabia inayofanywa na baadhi ya wazazi wanaodiriki kufanya mapenzi
na watoto wao wa kike ni lazima ilaaniwe duniani kote,ili kukomesha
vitendo hivyo vya aibu.
Alisema dunia ya leo imeharibika
kwani wapo wazazi ambao wanawabaka ama kuwafanya mapenzi watoto
waliowazaa wenyewe bila ya kuona aya.
Alieleza pia,vijana na
wazee(mashuga dadi) wanaokimbilia watoto wadogo waliopo mashuleni waache
tamaa za kimwili na atakaebainika atafungwa miaka 30 jela .
Mama Salma aliitaka jamii
kuheshimu na kujali watoto wa kike maana ni nguzo ya maendeleo ya taifa
,dhana potofu zikomeshwe zinazowanyanyapaa na kuwadhalilisha watoto wa
kike na ikumbukwe malezi na makuzi ya watoto wa kike ni wajibu kwa kila
mmoja kwenye jamii .
“Unavyoona huwezi kufanya mapenzi
na mtoto wako basi usijaribu kufanya mapenzi na mtoto wa jirani
yako,kwani mtoto wa mwenzio ni wako,”
Mama Salma aliwaambia wazazi na
walezi, watenge muda wa kuwafundisha kujikinga na majaribu wanayokutana
nayo kwenye mzunguko wa maisha yao,wawape haki za msingi zinazostahili
ikiwa ni sanjali na elimu sawa na watoto wa kiume.
Aliwaasa na wanafunzi wa kike
wakubaliane na hali ya maisha waliyonayo wazazi wao wasiwe na tamaa hali
inayosababisha kupata vishawishi.
Mama Salma,aliwahusia watoto hao
watumie stadi walizopatiwa kama silaha ya kujikinga na maadui hivyo
wasikubali kuzima ndoto zao na elimu .
“Someni msikimbilie kuolewa
,mtapata mnachokitaka hadi mtachoka,wanaume wapo tuu,serikali inahimiza
msome na kuwawekea misingi mizuri ya kielemu ikiwemo kusomeshwa bure,
acheni mchezo,jilindeni”
“Ni haki ya mtoto wa kike nae
kujilinda,ajitunze ili siku moja afikie ndoto zake kuwa
mwalimu,mainjinia ama madaktari bingwa.mawaziri, makamu wa rais”.
Mama Salma alielezea,kwasasa nchi
inajivunia kuwa na naibu katibu mkuu wa kwanza mwanamke wa umoja wa
mataifa kutoka Tanzania,Asharose Migiro ,makamu wa rais mwanamke wa
kwanza Samia Suluhu Hassan na waziri wa fedha wa kwanza Tanzania Zakia
Meghji.
“Wapo wengi nikiwataja hapa
hawatoshi ,hawa wametupa heshima na wamefika hapo kutoka na
elimu,jaribuni kufanya bidii mfikie malengo yenu,“Ninawausia ni lazima
kuienzi elimu kwanza,tunahitaji walimu kutoka nchini sio nje ya nchi,na
kuacha kubeza ualimu kuwa kwenda ualimu ni hadi ukose kazi nzuri
nyingine ,alifafanua Mama Salma.
Katika hatua nyingine alisema anaimani kutatiliwa mkazo kwa
kuingiza somo la stadi za maisha katika mtaala wa shule nchini ili
kujenga wasichana waweze kujisimamia na kujitambua wenyewe .
Mama Salma alisema,tumekuwa
tukijifunza mengi kupitia miradi mbalimbali ya kufundisha stadi za
maisha ikiwemo kupambana na mimba za utotoni.
Alitoa wito kwa wadau wa elimu
,halmashauri kuchangia changamoto hizo kwa kutenga bajeti za ujenzi wa
mabweni ya wanafunzi wa kike katika shule za sekondari”,Sanjali na
madarasa na maabara kwani itakuwa rahisi kuzungumza na mashirika
mbalimbali yasiyo ya kiserikali yaweze kusaidia kirahisi.
Nae mkuu wa wilaya ya
Kibaha,Assumpter Mshama ambae alimwakilisha mkuu wa mkoa huo,alisema
zipo baadhi ya mila na desturi zipo mkoani hapo ambazo zinachangiua
kukatisha masomo ya watoto kwa kuwaoza kabla ya kumaliza masomo yao.
Alisema utoro na mimba mkoani
Pwani ni sababu kubwa inayoshusha taaluma kwa watoto kijumla kwani kwa
mwaka huu watoto wa kike 61 wa darasa la saba mkoani hapo wamepata mimba
na kushindwa kufanya mitihani yao ya mwisho.
Assumpter alieleza ,utoro ni 58
,vifo sita na magonjwa ni 12 hivyo watoto watambue umuhi wa kujiendelea
kielimu kama ufunguo wao wa maisha.
Kwa upande wake,afisa elimu mkoa
wa Pwani ,Germana Sondoka alisema wataendelea kusimamia maelekezo ya
serikali na kimataifa ambayo yanahusika kumlinda mtoto wa kike ili aweze
kutimzia ndoto zake.
Alisema watahakikisha wanafunzi
mkoani humo hasa wa kike wanafikia malengo yao na kutokomeza vitendo
vinavyochangia kumkatisha mtoto huyo masomo yake.
Germana alieleza kufuatia
kaulimbiu ya kutokomeza mimba za utotoni kufikia uchumi wa viwanda
,watashirikiana baina ya serikali mkoa,maafisa elimu,walimu na wanafunzi
kwa kuendelea kuitafsiri kauli hiyo kwa vitendo.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la
kiserikali la Room To Read,wanatekeleza mradi wa kumwendeleza mtoto wa
kike ,Peter Mwamanga,alisema shirika hilo lilianza mwaka 2012 ambapo
wanafundisha pia stadi za maisha kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari.
Alisema mtoto wa kike amekuwa
akipambana na changamoto nyingi hadi kufanikiwa na kujikuta zipo
anazokutana nazo na kusababisha ndoto zake zikififia siku hadi siku.
Mwamanga alitoa wito kwa wadau
mbalimbali kushirikiana kutokomeza vitendo vya mimba za utotoni na
kupambana na wale wanaokatisha masomo ya watoto hao.
Room To Read walichukua fursa hiyo
kumpatia tuzo mama Salma ya kutambua na kuthamini mchango wake wa
kuwakomboa na kupambana kutetea haki za mtoto wa kike na mimba za
utotoni,kupitia WAMA.
No comments:
Post a Comment