Waziri wa nchi Ofisi ya Rais
Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika,
akizungumza jambo mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam
katika hafla ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo
Angellah Kairuki ambaye sasa amekuwa Waziri wa Madini
Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Menenjimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye sasa
amekuwa Waziri wa Madini Angelah Kairuki akielezea jambo mbele ya
waandishi wa habari katika hafla ya kumkabidhi ofisi mrithi wake Waziri
George Mkuchika leo Jijini Dar es Salaam .
Aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya
Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angelah Kairuki
akimkabidhi nyaraka za ofisi Waziri aliyeteuliwa kuongoza Wizara hiyo
George Mkuchika katika hafla iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya
Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angelah Kairuki
akielezea jambo mbele ya waandishi wa habari katika hafla ya
makabidhiano ya ofisi na waziri aliyeteuliwa kuongoza wizara hiyo George
Mkuchika leo jijini Dar es Salaam.
Picha na: Thobias Robert – MAELEZO
…………
Na: Thobias Robert- MAELEZO
11-10-2017
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema
kuwa atashughulikia suala la rushwa pamoja na udanganyifu wa umri
unaofanywa na baadhi ya watumishi wa umma hapa nchini.
Mkuchika aliyasema hayo Jijini
Dar es Salaam katika mkabidhiano ya Ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara
hiyo ambaye kwa sasa ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki katika
ukumbi wa wizara hiyo.
“Tutaongeza kasi ya kurejesha nidhamu, maadili na mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini,” alifafanua waziri Mkuchika
Katika hafla hiyo ambayo pia
ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Laurean Ndumbaro pamoja
na watumishi wa wizara hiyo, Waziri Mkuchika alisema kuwa atahakikisha
anashughulikia suala la watumishi kupandishwa madaraja pamoja na
kuongezewa mishahara baada ya kukamilika zoezi la ukaguzi la watumishi
hewa.
Aidha alisema kuwa suala la rushwa
linatakiwa kujengewa msingi kutoka ngazi ya chini, hivyo ataongea na
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ili kuweka
somo la rushwa katika mitaala ya elimu hapa nchini kuanzia shule ya
msingi hadi vyuo vikuu.
“Ukienda katika nchi ambazo
zimefanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa, mfano Norway, Sweden,
pamoja na mataifa ya Scandinavia utakuta wamefanikiwa kwasababu wananchi
wote wamepewa elimu dhidi ya rushwa na wanafahamu kwamba rushwa ni adui
wa haki, lakini tujiulize watanzania wangapi wanajua kuwa rushwa ni
adui wa haki, ni wachache tu,” alisema Waziri Mkuchika.
Aliongeza kuwa, makongamano,
semina pamoja na mikutano inayofanya na watumishi wa umma kwa wananchi
inapaswa ishirikishe Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU)
ili kutoa elimu juu ya rushwa na kujenga uelewa kwa wananchi kwani
itasaidia sana kumaliza tatizo la rushwa hapa nchini.
Waziri Mkuchika alimpongeza
mtangulizi wake na kuahidi kuendeleza jitihada alizokuwa akiendelea nazo
ikiwemo kuondoa watumishi hewa, vyeti feki, wanaoghushi umri pamoja na
uzembe wa wafanyakazi katika ofisi za umma hususani katika Halmashauri.
Kwa upande wake Waziri Kairuki,
aliwapongeza watumishi wa Idara, Wakala wa Serikali, Taasisi pamoja na
Wizara hiyo kwa ujumla kwa ushirikiano na ushauri walioutoa kwa muda
aliofanya nao kazi takribani miaka miwili kwa kuimarisha nidhamu,
maadili na kuondoa watumishi hewa katika ofisi za umma.
“Tumeweza kurejesha kwa kiasi
kikubwa nidhamu katika utumishi wa umma, tumeweza kwa kiasi kikubwa
kuanza kujenga misingi ya kuelekea katika kuboresha masilahi ya
watumishi umma maana ilikuwa ni lazima tuanze kusafisha kwanza lakini
pia tumeweza kuondoa watumishi hewa, pamoja na kuondoa watu ambao
hawakuwa na sifa stahiki katika utumishi wa umma,” alifafanua Waziri
Kairuki.
Waziri Mkuchika aliteuliwa kuwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala
Bora kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika baraza la mawaziri na Rais
wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ambapo
aliyekuwa anaongoza wizara hiyo Angelah Kairuki aliteuliwa kuwa waziri
wa madini.
No comments:
Post a Comment