Serikali yawataka watanzania
kurejesha nchi katika misingi iliyoachwa na Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuwa na viongozi waadilifu,wazalendo
na wenye uchungu na nchi yao.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar
es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. William
Ole Nasha wakati akifungua Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 18 ya Hayati
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ole Nasha amesema kuwa kumekuwa na
ombwe kubwa la kuporomoka kwa maadili, kushamiri kwa rushwa, ufisadi,
kukosekana kwa uzalendo na uwajibikaji, kuwepo kwa wafanyakazi hewa na
biashara ya madawa ya kulevya.
Ameongeza kuwa wengi waliokuwa wakiharibu nchi hii ni watanzania wenyewe kwa ajili ya tamaa na ubinafsi wao.
“Nimefarijika sana kusikia kuwa
Chuo kimeanza kurejesha hadhi yake iliyokuwepo hapo awali kilipoasisiwa
kwa kuanzisha program maalum ya Uongozi, Maadili na Utawala
Bora,”alisema Ole Nasha.
Akizungumzia Mada Kuu ya Kongamano
ambayo ni Mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika Uchumi wa Viwanda na
Maendeleo ya Jamii, Naibu Waziri amesema kuwa ni ukweli usiopingika
katika uchumi wa maendeleo ya viwanda, Uzalendo, Utaifa, Uadilifu na
Uongozi Bora vinapaswa kuzingatiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema kuwa
viwanda si maendeleo bali ni matokeo ya maendeleo.
Amesema nchi inawezakuwa na
viwanda lakini vinamilikiwa na wageni huku watanzania wakiwa manamba na
vibarua. Hivyo amewataka wananchi wenyewe wajitahidi kuanzisha viwanda
ambavyo vitatoa ajira kwa vijana wa kitanzania.
Butiku amesema kusema nchi imeendelea wakati bado kuna rushwa na kutokuwajibika huko sio kuendelea bado inahitaji kuendelea.
Akimzungumzia Mwalimu alisema kuwa
Nyerere alisema huwezi kujenga viwanda bila kujali misingi. Misingi
hiyo Butiku ameitaja kuwa ni kuhtambua kuwa Tanzania ni nchi ya
watanzania, usawa wa binadamu msingi ambao Mwalimu alikuwa muumini.
Jambo ambalo limejitokeza kwa wingi katika Kongamano hilo ni msisitizo ulikuwa juu uzalendo, utaifa,uadilifu na uwajibikaji.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na
wanataaluma, wananchi wa kawaida, wanafunzi, wanavyuo na viongozi
wastaafu akiwemo Spika wa Bunge Mstaafu, Anna Makinda, Ibrahim Kaduma,
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Mark
Mwandosa na Viongozi wa Vyama vya Siasa akiwemo Prof. Ibrahim Lipumba
na John Shibuda.
No comments:
Post a Comment