Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu amesema kuwa kata za Kigamboni, Vijibweni, Tungi zinatarajiwa
kupata umeme wa uhakika kufuatia kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa
kituo cha kupoza umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mgalu aliyasema hayo
tarehe 27 Novemba, 2017 kwenye ziara yake katika kituo cha kupoza umeme
Kigamboni na katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika kata za
Kisiju na Mkamba zilizopo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Alisema kituo hicho kitakuwa na
uwezo wa kuhudumia wateja kutoka 6,000 hadi 12,000 na kuongeza kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Nishati itahakikisha vituo vingine vya
kuboresha hali ya umeme ndani ya jiji la Dar es Salaam vinakamilika
mapema Desemba 15, 2017 na kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme mara
kwa mara lililokuwa linajitokeza.
Aidha, alilitaka Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) kukamilisha vituo vingine vilivyobaki vya
Kurasini, Gongo la Mboto na Mbagala mapema ili wakazi wa jiji la Dar es
Salaam waweze kuondokana na tatizo la ukosefu wa umeme.
Katika hatua nyingine, Mgalu
aliwataka wandarasi waliopewa kazi ya kujenga miundombinu ya kusambaza
umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha
miradi mapema na kuongeza kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi
atakayezembea ukamilishwaji wa mradi wake.
“ Wananchi wanahitaji umeme wa
uhakika na kwa gharama nafuu, umeme ndio uchumi wa nchi na kama Wizara
ya Nishati tupo kwa ajili ya kuhakikisha uchumi wa viwanda unakua kwa
kuhakikisha nishati ya umeme ya uhakika inapatikana sehemu zote hasa
vijijini,” alisisitiza Mgalu
Vilevile, Mgalu aliitaka REA
kuainisha vipaumbele katika usambazaji wa umeme vijijini, kipaumbele
kikiwa ni vijiji vyenye wakazi wengi na taasisi kama hospitali,
makanisa na misikiti.
Akizungumzia suala la fidia kwa
wakazi wanaopisha ujenzi wa miundombiniu ya umeme unaosimamiwa na REA,
Naibu Waziri Mgalu alisema hakuna fidia kwa kuwa serikali
imekwishagharamia gharama zote na kinachohitajika kwa wananchi ni
kulipia gharama za Kodi (VAT) ambayo ni shilingi 27,000.
Aliwataka wakazi wa Kata za Kisiju
na Mkamba wilayani Mkuranga kutandaza mifumo ya nyaya (wiring) kwenye
nyumba zao au kununua kifaa maalum cha Umeme Tayari (UMETA) mapema kwa
ajili ya kujiandaa na huduma ya umeme.
Akielezea mikakati ya Serikali
katika kuhakikisha umeme unapatikana hususan katika wilaya ya Mkuranga
yenye viwanda vingi, Naibu Waziri Mgalu alisema Serikali inatarajia
kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi Somanga Fungu na
kusambaza gesi nyingine kwenye viwanda vitakavyohitaji.
Aliongeza kuwa Serikali inatarajia
kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Stieglers
Gorge utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,100 na kukamilisha
miradi ya Kinyerezi II na Kinyerezi III
Alisema kuwa lengo la serikali ni
kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 Megawati 5,000 zinapatikana na nchi
kuingia kwenye uchumi wa viwanda utakaozalisha ajira kwa vijana hususan
kwa vijana waishio vijijini.
“ Tunataka mazao yasindikwe
vijijini na kusafirishwa ndani na nje ya nchi yakiwa kama bidhaa,
tunataka mtumie fursa ya umeme kwa ajili ya uchumi wa viwanda badala ya
matumizi ya majumbani tu,” alisema Mgalu.
Naye Mbunge wa Mkuranga ambaye ni
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega alimshukuru Naibu Waziri
Mgalu kwa ziara yake katika wilaya ya Mkuranga na kuongeza kuwa wananchi
wana matumaini makubwa ya umeme wa uhakika kwani wilaya hiyo imekuwa
na changamoto ya ukosefu wa umeme kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment