Serikali imezitaka Halmashauri
nchini kuimarisha ukusanyaji kodi hususani katika pango la ardhi na
kuachana na kodi ndogondogo ili kuweza kujiendesha zenyewe katika
shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza na watumishi wa
Manispaa ya Ubungo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mhe. Angelina Mabula alisema kuwa katika mfumo mpyawa kielekitroniki
ambao kwa sasa umewekwa katika Idara ya ardhi kwa lengo la kodi ya pango
la ardhi, ni mfumo rahisi kwa Manispaa zote nchini.
Katika ziara yake ya kikazi
inayoendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam Waziri Mabula aliwataka
watendaji wa Manispaa hiyo kuhakikisha wadaiwa sugu wapatao 300
wanafuatiliwa na kulipa madeni yao ili kuongeza mapato yatakayosaidia
kuendesha shughuli za manispaa ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi,
kulipa fidia kwa maeneo wanayohitaji kuyatwaa kwa shughuli za Manispaa.
“Bajeti yenu ni ndogo
ukilinganisha na wadaiwa sugu kwa Manispaa yenu mnawadai milioni 500 kwa
block ya kimara tu, mnaviwanja 2,1210 kwa hiyo mkidai kwa Manispaa
nzima mnaweza kupata pesa nyingi ambayo itawezesha shughuli za
Halmashauri kusonga mbele”, alisema Mhe. Mabula.
Mhe. Mabula aliwataka kuimarisha
zaidi katika kusimamia masharti ya utoaji hati na kuwachukulia hatua
watu waliojenga ovyo bila vibali vya ujenzi na kuwasihi waanze kuwasaka.
“Fedha zote ziko kwenye Idara hii
ya ardhi kiasi kwamba mkiweza kusimamia zoezi la ukusanyaji pango la
ardhi na utoaji wa hati kwa kufuata utaratibu sahihi, fedha hiyo
ingeweza kuleta mapato mengi sana”, alisisitiza Mhe. Mabula.
Aidha Naibu Waziri Mabula
aliwataka watendaji wa Manispaa hiyo kuhuisha Mabaraza ya Ardhi ya Kata
na kuwapa elimu kuhusu masuala ya migogoro ya ardhi, ambapo pia
aliwashukuru kwa kuweza kutatua migogoro 37 ya ardhi katika Manispaa ya
Ubungo kiasi ambacho wanaonyesha kuwa na mwelekeo katika kutatua
migogoro ya ardhi kwa haraka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Manispaa ya Ubungo Bw. John Kayombo alibainisha Upungufu wa Watumishi
katika Idara ya ardhi ambapo aliiomba Serikali kuwapatia watumishi ili
kukidhi mahitaji na kurahisha ufanisi wa kazi katika Manispaa hiyo.
Aliongeza kuwa Serikali itoe
suluhu katika migogoro ya mipaka kwa Wilaya hiyo ili kuwezesha
upatikanaji wa maeneo ya kutengeneza fursa kwa wa wakazi wa Manispaa ya
Ubungo.
No comments:
Post a Comment