Naibu Waziri wa Mifugo Abdallah Ulega, ametolea ufafanuzi suala la
vifaranga waliokamatwa wakiingizwa nchini kinyume na sheria na kuchomwa
moto, na kusema kwamba serikali ililazimu kufanya hivyo.
Akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast kinachorushwa na
East Africa Radio, Waziri Ulega amesema iwapo serikali isingechukua
uamuzi huo ingeleta madhara makubwa kwa nchi ikiwemo kuangamiza ndege
wafugwao wote na hata kupelekea vifo.
“Mafua ya ndege ni ugonjwa hatari sana tumeshuhudia hapo nyuma nchi
zenye maendeleo makubwa zilipata tatizo la mafua ya ndege, watu walikuwa
wanatembea wakiwa wamevaa mask, unajaribu kutafakari ikitokea jambo
kama hili limetokea kwenye nchi, ina maana ndege wafugwao wote itapaswa
waangamizwe, wote, kama kuna mtu ana biashara yake wote wanaangamizwa”,
amesema waziri Ulega.
Naibu Waziri huyo aliendelea kwa kufafanua kuwa vifaranga hivyo
havikurudishwa kule vilikotoka kama ambavyo baadhi ya watu walikuwa
wakihoji, na kusema kwamba muhusika hakuwa na kibali, na iwapo
vingerudishwa na kuja kutokea tatizo, lawama zote zingekuwa kwa nchi ya
Tanzania.
“Watalam walimuuliza muhusika kama ana kibali akasema hana, na kama hana
taratbu ziko wazi, na kuna sheria ambazo zinawaongoza, ukisema
umrudishie alafu ikigeuka wakisema vinatoka Tanzania na bahati mbaya
ikaonekana vina maradhi na wakautangazia ulimwengu, sisi tungekuwa
tumebeba mzigo mkubwa ", amesema Mheshimiwa Ulega.
Naibu Waziri huyo amendelea kwa kusema kwamba inashangaza kwa mtu
kuingiza vifaranga kutoka nje ya nchi wakati kuna vifaranga ambao
wanazalishwa hapa ndani, na wanakosa soko.
No comments:
Post a Comment