• Breaking News

    ..

    ..

    Monday, 6 November 2017

    Paul Chaulo: KUWA OMBAOMBA SI JAMBO JEMA KIBINADAMU

    images
    Na Ali Issa Maelezo
    Suala la ombaomba kwa binaadamu ni baya na halifai kulifanya Mtu kwani linamuondolea hadhi na heshima kwa wezake na kupelekea kudharaulika.
    Hayo yamesemwa leo huko Jumuiya ya watu wenye ulemavu Zanzibar UWZ na Meneja wa Hoteli ya Serena Zanzibar Paul Chaulo wakati alipokuwa akikabidhi mifuko ya Saruji 20 kwa kikundi cha watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na kilimo cha mbogamboga na ufugaji katika shehia ya dole wilaya ya magharibi A Unguja.
    Alisema utowaji wa saruji hiyo ni kuwawezesha walemavu wa kikundi hicho kujenga mabanda ya ufugaji wa kuku na ngombe wa maziwa na kuendeleza kilimo cha mboga mboga pale mtaji wao utakapo kidhi mahitaji.
    Amesema kuwa ulemavu sisababu yakumfanya mtu kuwa ombaomba bali ni kujikubalisha kujituma, kufanyakazi na kupata kipato cha halali kitu ambacho kitamjengea kupata heshima na kuondokana na dhana mbaya  ya ombaomba.
    Amesema msaada wao mdogo waliotoa ni hatua yamwanzo ambayo itawasaidia kuanzisha shughuli zao na wameahidi kusaidia Zaidi pale watakapoona  wamefanya vizuri.
    “Nimewapa hiki kidogo kwa kuazia imani yangu mtakitumia vizuri kuendeleza malengo yenu, mtoto anaaza hatua moja na kusonga mbele, iwapo mtafanya vizuri nitakuja tena kuwaona,”alisema meneja huyo Chaulo.
    Aidha aliwaeleza kuwa iwapo wataitumia vizuri msaada huo ameahidi kuwa mlezi wa kikundi hicho na kukipa kila aina ya misaada ikiwemo kuwatafutia soko la mazao yao watakayozalisha katika ushirika wao.
    Nae Mkururugenzi wa Jumuiya ya Watu wenye ulemavu Zanzinbar (UWZ) Asia A. Hussen alimshukuru Meneja huyo na uongozi mzima wa Hoteli ya Serena kwa msaada wao kwa kikundi hicho cha walemavu wa viungo na kuwaomba msaada huo usiishie hapo bali waendelee kusaidia vikundi vyengine kwani kuwawezesha walemavu ni kuisaidia Jamii hiyo ambayo inahitaji msukumo mkubwa.
    Alisema kunaidadi kubwa ya vikundi vya ushirika vya walemavu na baadhi yao wameanza kuzalisha lakini wanashindwa kupata soko la uhakika kuuza mazao yao.
    Mkurugenzi huyo alimuomba Meneja kuwasaidia kupatia masoko kwa vile bidhaa wanayo zalisha zinahitajika katika Hoteli zao, ombi ambalo meneja alilikubali.
    Nae Mwenyekiti wa kikundi cha kilimo cha mboga mboga na ufugaji Shehia ya Dole Mwichande Haroun akipokea msaada huo aliushukuru uongozi wa Serena Zanzibar na kusema umekuja wakati muafaka na watautumia kama ilivyo kusudiwa.
    Alimuomba meneja kupanga siku kwenda kuona jitihada zao za awali juu ya msaada huo ulivyotumika .
    Aidha Mwenyekiti huyo alieleza kuwa kikundi chao kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo uhaba wa fedha kwani wanampango wa kuwa na mradi mkubwa zaidi hapo baadae.
    Alisema fedha chache walizopata kuanzisha kilimo cha mboga mboga zimepatikana kutokana na michango ya wanakikundi wenyewe ambao ni wanyonge na wanahitaji kusaidiwa.
    Mwenyekiti huyo aliomba wafadhili wengine wajitokeze kusaidia kikundi hicho cha ushirika ili kiweze kupiga hatua za maendeleo.
    Hata hivyo Mwenyekiti huyo aliwataka walemavu wa viungo wanaopenda kujiunga na kikundi hicho wajitokeze ili kuimarisha kikundi hicho.
    Kikundi cha kilimo cha mboga mboga cha walemavu shehia ya dole kwa sasa kina wanachama tisa wakiwemo wanawake wawili na kimeazishwa mwaka jana.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI