SIKU moja baada ya gazeti hili kuchapisha makala kuhusu mateso yanayompata mtoto Wilson Jackson (11), mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam anayeteseka kitandani kwa miezi sita sasa baada ya kupata ajali ya kugongwa na lori aina ya Mitsubishi Fusso, wasamaria wameanza kujitokeza kumsaidia mtoto huyo.
Jana msamaria, ambaye hata hivyo hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alijitokeza na kumchangia mtoto huyo Sh milioni moja za matibabu, akieleza kuguswa na mateso ya mtoto huyo.
Fedha hizo zilikabidhiwa kwa baba wa mtoto huyo, Jackson Ngowo na Kaimu Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Kampuni inayochapisha gazeti hili ya Tanzania Standard Newspapers Limited (TSN), Mkuu Akida.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano ya fedha hizo, Naibu Mhariri Mtendaji wa TSN, Tuma Abdallah alisema TSN kupitia magazeti yake, wataendelea kuhamasisha jamii kujitokeza ili kumsaidia mtoto huyo ili afya yake irejee.
“Vyombo vyetu vya habari vitaendelea kuhamasisha jamii kutoa michango yao ya kusaidia matibabu ya mtoto Wilson. Ni imani yetu kuwa fedha hizi zilizopatikana zitaendelea kulipia gharama za matibabu ya mtoto ambayo yalikuwa yamekwama,” alisema Tuma.
Kwa upande wake, Ngowo aliishukuru TSN na msamaria aliyejitokeza kusaidia. Alisema fedha hizo atazitumia katika matibabu na lishe ya mtoto ili kutimiza lengo la kuokoa maisha ya mwanawe.
“ Niwashukuru ninyi, nimshukuru aliyenisaidia katika kutetea maisha ya mwanangu, nimehangaika sana kupigania maisha ya kijana wangu na hali kwangu ilikuwa mbaya, fedha hizi nitazitumia kwa lengo la matibabu ya mwanangu na si vinginevyo,” alisema.
Wilson akiwa na kaka yake, Ibrahim (15) walipata ajali Februari 28, mwaka huu huko Mpiji Magohe baada ya kugongwa na Fusso.
Ajali hiyo ilisababisha Ibrahim kuvunjika mfupa wa paja na Wilson kupata matatizo kwenye kichwa na ubongo, hali ambayo imeathiri mishipa inayounganisha kichwa na uti wa mgongo na kuathiri pia uwezo wake wa kutoa sauti.
Wilson anahitaji nepi maalumu, lishe na zaidi matibabu ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida. Pia anahitaji kiti cha magurudumu kitakachosaidia kumkalisha ili kunyoosha viungo.
Jamii inaombwa kumsaidia kupitia simu namba 0652 255 942 ( Jackson Ngowo) au 0742 731 878 (Neema Ndosi).
Aliyeguswa pia anaweza kumchangia chochote mtoto huyu kupitia Mhariri wa gazeti hili kwa namba 0766 843 382 jina Nicodemus Ikonko
No comments:
Post a Comment