• Breaking News

    ..

    ..

    Monday, 5 September 2016

    TMA: Mvua za vuli zitachelewa



    MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imetahadharisha kuchelewa kwa mvua za vuli na kusema hata zitakazonyesha, zitakuwa ni za wastani au chini ya wastani katika maeneo mengi ya nchi katika kipindi kinachoanzia Oktoba hadi Desemba, mwaka huu.
    Aidha, imesema kuanza kwa vuli kunatarajiwa kuwa na vipindi vikavu katika maeneo mengi hususan katika miezi ya Oktoba na Novemba. Imesema kutokana na hali hiyo, hali ya unyevunyevu katika udongo inatarajia kuwa si ya kuridhisha kwa ustawishaji wa mazao ya kilimo na malisho kwa mifugo.
    Imewashauri wakulima kuandaa mashamba na pembejeo mapema pamoja na kuzingatia ushauri wa maofisa ugani wa kilimo kwa matumizi sahihi ya ardhi na mbegu, pia kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula walichonacho.
    Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mwelekeo wa msimu wa mvua nchini kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba, mwaka huu.
    Kuhusu hali ya mifumo ya hali ya hewa alisema hali ya joto la chini ya wastani iliyopo katikati mwa eneo la kiikweta la Bahari ya Pasifiki na Magharibi mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Afrika Mashariki) inatarajiwa kuendelea kuwepo katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba.
    Alisema katika eneo la Mashariki mwa Bahari ya Hindi hali ya joto la juu ya wastani iliyopo inatarajiwa kuendelea katika kipindi cha msimu wa vuli.
    “Hali ya mfumo wa joto inaashiria kuwepo kwa upepo wenye unyevunyevu hafifu kutoka Mashariki kuelekea Pwani ya Afrika Mashariki,” alisema Dk Kijazi na kuongeza kuwa hali hiyo ya joto la chini ya wastani katika Bahari ya Pasifiki imepewa jina la La Nina yaani mvua chini ya wastani.
    Alisema hali hiyo ya mfumo huo wa upepo, unatarajiwa kusababisha upungufu wa mvua katika maeneo ya Kaskazini na yale ya Kaskazini –Mashariki mwa nchi, huku katika eneo la Magharibi mwa Bahari ya Hindi, joto la wastani linatarajiwa kuwepo kuelekea mwezi Desemba na hivyo kusababisha kuchelewa kuanza kwa mvua katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI